Viongozi wa chama cha upinzani cha Cord wamekashifiwa kutokana na matamshi waliyotoa wakati wa mkutano katika bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi.
Mwenyekiti wa chama cha TNA tawi la Nakuru Dkt Abdul Noor, alimkemea Seneta wa Machakos Johnston Muthama, kwa kusema kuwa alimkosea heshima Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta kwa kutoa hotuba iliyo sheheni ubinafsi.
Akiongea mjini Nakuru siku ya Ijumaa, wiki iliyopita, Dkt Noor alisema seneta huyo alifaa kuchunga ulimi wake kabla ya kutoa matamshi aliyotoa kuhusu Rais na Waziri wa Ugatuzi Bii Ann Waiguru ikizingatiwa alikuwa kwenye runinga za kitaifa.
“Waliita mkutano kuzungumzia maswala ya mgomo wa walimu, hivyo ndivyo wangefanya. Matamshi yake yaliashiria mtu ambaye si kiongozi na anayetaka kuleta mgawanyiko katika taifa hili,” alisema Noor.
Noor alitoa wito kwa NCIC, kushirikiana na ofisi ya DPP na kumchukulia hatua Muthama ili iwe funzo kwa wanasiasa wengine nchini dhidi ya kutoa matamshi ya kiholela.
“Wakati ambapo tunaombea usalama wa taifa kila uchao, wengine wako mbioni kutugawanya. Akichukuliwa hatua na NCIC, itakuwa bora ili kesho akitoa hotuba awe mwangalifu,” alisema Noor.