Naibu wa Gavana kaunti ya Uasin Gishu Daniel Chemno aliwaongoza viongozi wengine katika kaunti hiyo kukutana na wananchi kujadili baadhi ya maendeleo waliyoyafanya tangu kuchaguliwa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Chemno alisema kuwa ingawaje serikali za kaunti zimekuwa na changamoto wao wameweza kutimiza baadhi ya ahadi walizo waahidi wananchi wa kaunti hiyo.

Naibu wa gavana huyo aliongeza kusema kuwa serikali hiyo itaendelea kufanyia wananchi kazi ili kuinua maisha yao.

"Kwa sasa tumefaulu kutenga Sh90 milioni ili kuwasomesha wanafunzi kutoka familia zisizojiweza ili kulipa karo ya vyuo vikuu na shule za sekondari," alisema Chemno..

Aliendelea kusema kuwa asilimia 70 ya pesa hizo husaidia wanafunzi walioko katika shule za upili ambao ndio wengi ilhali asilimia 30 huenda kwa wale walioko katika masomo ya juu.

Aliongeza kuwa serikali ya kaunti hiyo inawasomesha wanafunzi 600 kila mwaka katika shule ya Rifty Vallet Technical Training Institute (RVTTI) iliyoko mjini Eldoret ili wapate ujuzi unaokosekana katika jamii.

Kwingineko naibu wa gavana huyo alieleza kuwa wizara ya afya ya kaunti hiyo inatazamia kuajiri wahudumu wa afya 360 .

Richard Etyang’ mkaazi wa kaunti ya Uasin Gishu alionesha kutoridhika kwake na jinsi serikali hiyo inavyo ajiri watu kwa njia ya kikabila ilhali kaunti hiyo ina watu wa kabila na matabaka mbali mbali.

“Kaunti hii ina watu wa kabila mbalimbali lakini nasikitika kueleza kuwa watu wa kabila moja tu ndio hupata ajira hapa. Naomba kaunti kushughulikia jambo hili kwa undani,” alisema Etyang

Alimwomba Chemno kushughulikia ombi lake na kuajiri watu kulingana na ufuzi wala sio kulingana na kabila.