Viongozi wa kaunti ya Mombasa na ukanda wa Pwani kwa jumla wametakiwa kuingilia kati vita dhidi ya mihadarati.
Akiongea katika eneo la Mtopanga huko Kisauni mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Kisauni Julius Kavita amesema kwamba licha ya kuwa janga la mihadarati limeikumba zaidi ukanda wa Pwani hususan kaunti ya Mombasa viongozi hawajaonekana kujitokeza kuongelea swala hilo.
Aidha afisa huyo wa utawala amewakashifu wanasiasa wa kaunti ya Mombasa kwa kuendeleza siasa badala ya kuzungumzia janga linaloathiri jamii
Amewataka wananchi na washikadau mbalimbali kushirikiana kikamilifu na serikali ili kulikabili janga hilo la mihadarati ambalo limekuwa sugu katika ukanda wa Pwani.
"Tafadhalini wananchi hakikisha kuwa mnashirikiana na serikali katika kupiga vita mihadarati na pia lazima viongozi wajitokeza kuhakikisha kuwa swala la mihadarati Mombasa linakomwe,” alisema Kavita.
Kauli yake inajiri huku utumizi wa mihadarati ukitajwa kuongezeka katika kaunti ya Mombasa.