Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa bunge la kaunti ya Mombasa wameshtumu hatua ya tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, ya kudhalilisha kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kufuatia kashfa ya ufisadi ya Eurobond.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya uhasibu wa fedha za umma katika kaunti hiyo Fadhil Mwalimu, kwenye kikao na wanahabari mjini mombasa siku ya Ijumaa, wamesema kwamba tume ya EACC ina mamlaka kikatiba kuchunguza ripoti wanayopewa na kuwachukulia hatua wahusika, lakini cha kustajabisha ni kuwa tume hiyo imebadili mwelekeo na kuwachunguza wanaotoa habari muhimu kwao.

Mwalimu amesema kwamba kiongozi huyo anafaa kuheshimu kutokana na jinsi alivyochangia kuleta demokrasia na uhuru wa kujieleza nchini kwa mujibu wa katiba ya nchi, huku akidai kuwa serikali ya Jubilee imedhihirisha wazi kuwa imeshindwa kukabiliana na ufisadi nchini.

Kiongozi huyo ameunga mkono hatua ya Raila Odinga ya kudinda kufika mbele ya tume ya EACC, akisema kwamba Raila anafaa kupewa heshima kama viongozi wengine wakuu serikalini kutokana na juhudi zake za kubadilisha uongozi wa taifa hili na kuwatetea Wakenya.

"Sisi kama viongozi wa kaunti ya Mombasa na wanachama wa chama cha ODM tunamuunga mkono kiongozi wetu Raila Odinga kwa kudinda kwenda mbele ya tume ya EACC na iwapo wanalazima basi maafisa wa tume hiyo wafike katika afisi ya Raila," alisema Mwalimu. 

Haya yamejiri huku viongozi mbalimbali katika kaunti ya Mombasa akiwemo gavana wa kaunti hiyo Hassan Ali Joho wakishtumu hatua iliyochukua tume ya EACC dhidi ya Raila Odinga.