Viongozi wa Pwani waliyouasi mrengo wa Cord wamewashtumu vinara wa mrengo huo kwa kulumbana hadharani juu ya nani atakayeongoza mrengo huu wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Wakizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, viongozi hao wamesema kuwa kulumbana kwa vinara wa mrengo huu kunaonyesha wazi kuwa ni viongozi waliyo na tamaa ya uongozi na wala hawana azma yoyote ya kuwaunganisha Wakenya na kuwafanyia maendeleo.
Wakiongozwa na Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro, wamekabla viongozi hao kuungana wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka wa 2013 walisaini mkataba wa maelewano kuwa mwaka wa 2017 mrengo huo utaongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.
Mung’aro aidha amewataka wakaazi wa Pwani na Wakenya kwa jumla kuhakikisha kuwa wanadumisha amani na kutangamana kama jamii moja ili kuondoa chuki, ukabila na maswala ya kidini ambayo huwatenganisha Wakenya kwani azma ya vinara wa mrengo wa Cord sasa ni kuwagonganisha Wakenya.
“Sisi kama viongozi wa Pwani tunaona Vinara hawa wa Cord wanamalengo potovu ya kuwatenganisha Wakenya kwa sasa, kama walikubaliana mbona sasa wanagonganisha Wakenya? hiyo ni kumaanisha wanatamaa ya uongozi na wala sio kuwafanyania Wakenya maendeeleo, hatua kama hiyo sio demokrasia wanaoyosema,” alisema Mung’aro.
Viongozi hao sasa wanasema kuwa wataunga mkono mrengo wa Jubilee katika uchaguzi mkuu ujao ili kuhakikisha kuwa wakenya na hususan wakaazi wa pwani wanapata maendeleo jinsi wanavyotarajia.
Kauli ya Mung’aro imeungwa mkono na Mbunge wa Kilifi Kusini Mustafa Idd, Mbunge wa Taveta Naomi Shaban, mwakilishi wa wanawake kaunti ya Kwale Zainab Chidzuga miongoni mwa viongozi wengine.