Idara ya Usalama katika Kaunti ya Mombasa imetoa onyo kali kwa viongozi wa kisiasa wanaotumia matamshi ya uchochezi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed amesema kuwa wanasiasa wenye nia ya kuwagawanya wakaazi kwa misingi ya kikabila na vyama na kusababisha ukosefu wa usalama watakabiliwa kisheria.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Maalim alisema kuwa idara ya usalama kamwe haitalegeza msimamo wake wa kuimarisha usalama, huku akisisitiza kuwa viongozi wachochezi watakabiliwa.

Kamishna huyo alisema kuwa msimamo wa serikali na idara ya usalama ni kuhakikisha kuwa taifa liko salama na lazima migogoro kusitishwa ili kuzuia kushuhudiwa kwa machafuko.

Wakati huo huo, amewataka Wakenya kujiepusha na viongozi wanaowachochea na wenye nia ya kuwagawanya kwa misingi ya kikabila ama kisiasa.

Alisema kuwa kila Mkenya ana haki kuishi popote nchini na idara ya usalama itahakikisha usalama unaimarishwa.

“Serikali iko tayari kuhakikisha kuwa usalama wa Wakenya unalindwa na viongozi wanaochochea Wakenya kikabila na kisiasa wanakabiliwa kisheria,” alisema Maalim.