Idara ya usalama katika ukanda wa Pwani imetakiwa kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa kisiasa wanaowaamuru walinzi wao kutumia mamlaka yao vibaya na kuwanyanyasa wananchi kwa malengo ya kupata umaarufu wa kisiasa.
Mchanganuzi wa maswala ya kisiasa katika eneo la Pwani Wakili Johnson Muchiri, amesema kuwa japo idara ya usalama mara nyingi ukiuka mwongozo na sheria za kiusalama, taifa hili linasheria na mwongozo wa katiba hivyo basi viongozi kama hao wanafaa kuchukuliwa hatua.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Ijumaa mjini Mombasa, Muchiri alisema kuwa tukio la hivi majuzi lililoshuhudiwa kwenye uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi ni la kusikitisha mno.
Alisema kuwa walinzi hao wa viongozi wakuu katika chama cha ODM wanafaa kuchukuliwa hatua kwa kuwa walinzi wanafaa kuhakikisha kuna usalama na wala sio kuwakandamiza wananchi.
Akizungumzia swala Gavana wa Mombasa Hassa Joho kupokonywa walinzi wake, Muchiri alisema kuwa la msingi ni gavana huyo kukubali kuwa walinzi wake walivunja sheria.
“Kuadhibiwa kwa Joho huenda ikawa ishara kuwa madai yanayosemwa ni ya kweli. Anafaa kuadhibiwa kwa kuponywa walinzi kwa muda kisha warudishwe kwa kuwa yeye ni kiongozi na anastahili kupewa uongozi,” alisema Muchiri.
Hata hivyo, alishinikiza idara ya usalama kuhakikisha kuwa wanawapa wananchi ulinzi dhabiti hasaa mashinani ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaishi kwa amani na utangamano.
Kuali ya Muchiri inajiri baada ya Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kupokonywa walinzi wake, agizo linalodaiwa kutoka kwa idara ya usalama Pwani, kufuatia shinikiza kutoka kwa Mshirikishi mkuu wa usalama kanda ya Pwani Nelson Marwa.