Viongozi wa Kisiasa katika kaunti ya Mombasa wametakiwa kuwaunganisha vijana na akina mama badala ya kuwachochea kuzua vurugu kwa manufaa yao binafsi.
Kiongozi wa wanawake katika eneo la Likoni Mildred Odinga amesema kuwa jamii imechoshwa na jinsi baadhi ya viongozi wa kisiasa wanavyowachochea vijana wadogo kuzua vurugu.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne katika mkutano wa wanawake, Odinga alisema kuwa lazima viongozi kama hao kusitisha uchochezi na kuwapa fursa waumini wa dini ya Kiislam kutekeleza saum yao kwa amani ili Kaunti ya Mombasa kudumisha amani.
"Tunawaomba viongozi wa kisiasa wasitishe siasa za kuwachochea vijana wadogo kuzua vurugu na kuharibu usalama kwa manufaa yao binafsi ili Kaunti ya Mombasa kuwa salama,” alisema Odinga.
Wakati huo huo, amewataka vijana kujitenga na viongozi kama hao na kuimarisha usalama wa kaunti, kwa kusema kuwa vijana ndio tegemeo la siku za usoni.