Viongozi wa kisiasa nchini wametakiwa kukoma kuwahusisha wananchi katika siasa za chuki na uchochozi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, katika mkutano na wanahabari, Katibu Mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa, alisema kuwa hatua hiyo huenda ikaleta uhasama mkubwa nchini na kusababisha vurugu.

Sheikh Khalifa aliukosoa mrengo wa Cord kwa kutumia uwezo wao wa kisiasa kushinikiza kubanduliwa kwa Tume Huru ya Uchuguzi na Mipaka IEBC.

Alisema kuwa hatua hiyo huenda ikachangia Wakenya kutokuwa na imani na tume hiyo, hali aliyosema huenda ikasababisha machafuko wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Sheikh Khalifa alisema kuwa njia pekee ya kufanya mabadiliko katika idara mbali mbali za serikali ni kupitia njia ya maelewano na mazungumzo ya busara yenye kuwaunganisha Wakenya wote.

"Tunawaomba viongozi wa kisiasa kutumia wakati wao vyema kwa kuwaunganisha Wakenya badala ya wao kutumia mamlaka yao vibaya na kusababisha uhasama utakaochangia machafuko wakati wa uchaguzi mkuu ujao,” alisema Sheikh Khalifa.