Viongozi wakidini katika kaunti ya Nakuru wameuliza viongozi wa kisiasa kuungana ili kukabiliana na changamoto zinazokabili taifa la Kenya, miaka 51 baada ya kujinyakulia uhuru.

Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi hao wa makanisa wakiongea katika eneo la Elburgon wametaja siasa potovu, ufisadi pamoja na donda ndugu la ukabila kama baadhi ya matatizo ambayo yameadhiri ukuaji na ustawi wa kiuchumi wa nchi hii.

Wamesema taifa la Kenya likilinganishwa na mataifa mengine ya ulimwengu ni taifa ambalo mwenyezi Mungu amebariki kwa udongo wenye rutuba pamoja na hewa safi inayoimarisha kilimo.

Wakiongozwa na mhubiri Kamuri Muya, wahubiri hao wamewataka wanasiasa kuweka tofauti zao kado na badala yake kuwatumikia wananchi wote bila kuwatenga kwa misingi ya kidini, kikabila, kimaumbile ama kimaeneo.

Muya ameuliza viongozi wa mrengo wa cord, mashirika ya kijamii pamoja na viongozi wa jubilee kudumisha uzalendo wanapotekeleza majukumu yao, na pia kupunguza tofauti zao ambazo zinaendelea kuwatenganisha wakenya.

Amesema mswada kuhusu usalama wa taifa na ambao umezua mdahalo mkubwa nchini unapaswa kushirikisha wadau wote ili idara ya usalama iweze kuendeleza juhudi zake za kukabiliana na magaidi wa Al shabab pamoja na makundi ya wahalifu waliojihami.

Mswada huo umeonekana kuzua tofauti kubwa katika ya viongozi wanaounga serikali, masharika ya kutetea haki za kibinadamu pamoja na mrengo wa cord huku majimbizano makali yakishuhudiwa katika bunge la kitaifa wakati hoja hiyo ilipokuwa ikijadiliwa mwishoni mwa juma.