Viongozi wa Kaunti ya Mombasa wametishia kufanya maandamano makubwa kupinga kile walichokitaja kama ongezeko la visa vya mauaji ya kiholela.
Viongozi hao walidai kuwa mauaji hayo yanatekelezwa na maafisa wa usalama.
Wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho, viongozi hao walisema kwa ushirikiano na mashirika ya kutetea haki za binadamu, wamevinakili zaidi ya visa 200 vya vijana wenye umri mdogo kuuawa kiholela, na wengine kupotea katika hali za kutatanisha.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Joho alisema kuwa mauaji ya aina hiyo yanastahili kukomeshwa ili kuwapa ulinzi dhabiti wakaazi wa kaunti ya Mombasa.
“Tumechoshwa na mauaji ya kiholela na kupotezwa kwa vijana wetu kila mara katika hali ya kutatanisha. Wanaofanya hivi sio wengine bali ni maafisa wa polisi. Tutafanya maandamano kukashifu hatua hiyo,” alisema Joho.
Kiongozi huyo wa kaunti amewalaumu maafisa wa usalama kwa ukiukaji wa haki za binadamu, akisema wengi wa wale ambao huuawa huwa hawana hatia zozote.
Kauli ya Joho inajiri baada ya kuuwawa kwa Salim Bedzimba eneo la Kisauni siku ya Alhamisi na mwenzake Kibwana Ahmed Abdallah al maarufu Rajab, kwa kushukiwa kuwa wafuasi wa kundi la ugaidi la al-Shabaab.