Kiongozi wa muugano wa Cord Raila Odinga amepewa changamoto kushirikiana na kiongozi wa chama cha Amani Musalia Mudavadi huku uchanguzi mkuu wa mwaka wa 2017 unapokaribia.
Himizo hilo limetolewa na aliyekuwa Meya wa Nairobi George Aladwa, Mbunge wa zamani wa Makadara Reuben Ndolo, Mbuge wa Dagorreti Kaskazini Simba Arati na Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa, waliokuwa wakizungumza siku ya Jumapili kwenye hafla ya maombi ya muungano wa COTU mjini Nairobi.
"Nataka kuwapa changamoto ndugu zangu Musalia na Odinga kuja pamoja ili tuweze kuunda muungano kabla ya uchaguzi wa 2017. Mulifanya kazi pamoja hapo awali na sioni sababu yoyote ya kuwazuia kuungana tena," alisema Bw Aladwa.
Aliongeza: "Tunahitaji watu wa jamii ya waluhya kuungana ili tusifanye makosa ya kugawanya kura za magharibi mwa Kenya. Tunahitaji kuwaokoa watu wa Kenya kutoka kwa utawala mbovu na hilo litaafikiwa iwapo tutaungana.”
Bwana Arati na Ndolo waliunga mkono usemi huo na kusema kwamba wawili hao wanapaswa kuweka tofauti zao za hapo awali kando, na kuunda muungano utaochukua ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.
"Ndugu yangu Musalia bado ni kijana na ombi letu ni kwamba aweke azimio lake kando na kumpa Raila nafasi ya kuwania urais. Nina uhakika kuwa Bwana Raila atamunga mkono wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022,” alisema Arati.
Bi Jumwa kwa upande wake alimtaka Bw Odinga kuunda muungano na viongozi wenye nia sawa ili kushinikiza usawa na ukuaji wa uchumi.
"Nchi yetu inahitaji watu kama Raila kushinikiza usawa na maendeleo. Tunatoa wito kwa Wakenya wenye nia sawa kujiunga na timu yetu ili tupate njia bora ya kusonga mbele,” alisema Juma.
Hata hivyo, Odinga na Mudavadi walikwepa mada hiyo walipotoa hotuba zao, huku Raila akitoa changamoto kwa serikali ya Jubilee kuanza mchakato wa upatanishi kote nchini miongoni mwa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.