Hata baada ya visa kadhaa vya moto kutokea katika kaunti ya Nyamira, bado serikali hiyo haijasoma lolote wala kuchukuwa hatua za kudhibithi janga hilo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kisa cha kuchomeka kwa bweni la shule ya Nyansabakwa ni cha nne mwaka huu baada ya mamilioni ya pesa kuteketea baada ya maduka kuchomeka katika soko la kebirigo, bweni kuteketea katika shule ya malezi ya Eronge na bweni lingine kuteketea katika shule ya upili ya Omoyo mapema mwaka huu. 

Kulingana na Samuel Ombui, ambaye ni Mkaazi wa mji wa Nyamira, serikali ya kaunti hiyo inatumia pesa nyingi kupeana msaada wa dharura kwa waathiriwa kuliko kutafuta suluhu la kudumu.

"Hii serikali inatumia pesa zetu kiholela, kila mara inakimbiza misaada ya dharura kwa waathiriwa tunaambiwa millioni mbili, milioni moja laki saba kwani hizo pesa haiwezi kununua magari ya kuzima moto? " amesema Ombui.

Mapema mwaka huu, gavana wa kaunti hiyo alinakiliwa akisema serikali hiyo ilikuwa imetoa zabuni ya ununuzi wa vifaa vya kuzima moto ambavyo vingefika katika kaunti hiyo Kwa muda mfupi.

"Tunatarajia vifaa vya kuzima moto kwa muda wa miezi miwili ijayo kwani tayari tishalipia kila kitu," alisema Nyagarama wakati huo.

Hata hivyo, baada ya kisa cha moto kuteketeza mamilioni ya mali kebirigo mwezi jana, Nyagarama alisema kuwa zabuni ya ununuzi wa gari la kuzima moto lilitupiliwa mbali kwani serikali hiyo ilikuwa imetenga shilingi millioni 30 ambazo hazingetosha kwani gari hilo lilikuwa linauzwa millioni 57.

Kwa hivi sasa ikiwa mkasa zaidi utatokea basi itabidi serikali hiyo kuomba msaada kutoka kaunti jirani ya Kisii.