Visa 20 vipya vya ugonjwa wa kipindupindu vimeripotiwa katika Kaunti za Baringo na Nakuru.
Visa hivyo vimeripotiwa katika maeneo bunge ya Rongai na Mogotio ambapo wanawake 11 wameathiriwa huku wanaume tisa wakiripotiwa kuwa na ugonjwa huo.
Kundi la maafisa wa sekta ya afya kutoka kaunti hizo mbili lilifanya mkutano wa majadiliano siku ya Jumanne ili kubuni mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo katika kaunti hizo.
Akiongea na wanahabari katika Kituo cha kiafya cha Mogotio ambapo watu 12 walio na ugonjwa huo wamelazwa, Mkurugenzi wa afya ya uma kwenye kaunti ya Nakuru Dkt Joseph Lenai alisema walio na ugonjwa huo wako chini ya uangalizi wa madaktari.
Dkt Lenai alisema kwamba kisa cha kwanza kiliripotiwa tarehe Septemba 17, 2015 lakini mgonjwa huyo alifika hospitalini tarehe Septemba 23.
“Tumekuwa tukifanya mikutano tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa wa kipindupindu kiliporipotiwa tarehe Septemba 17. Kumekuwa na visa ambavyo vimeripotiwa na vingine kudhibitishwa kuwa ni vya ugonjwa wa kipindupindu. Kundi la kudhibiti ugonjwa huo limekuwa likizunguka katika miji tofauti likiangalia njia za kuzuia ugonjwa huo,” alisema Dkt Lenai.
Hata hivyo, alidhibitisha kuwa hakuna maafa yoyote ambayo yameripotiwa kwa sasa kutokana na ugonjwa huo, akiongeza kuwa wameagiza kundi la kudhibiti ugonjwa huo katika vijiji mbalimbali huku wakiwa na lengo la kuwapa elimu wakazi wa vijiji hivyo kuhusiana na haja ya kunywa maji yaliyotibiwa na pia kutojisaidia hadharani.
Lenai alisema uwepo wa misala michache inayozingira mto wa Molo umepelekea maji kupata vijidudu vinavyosababisha ugonjwa huo, hatua ambayo imepelekea wakazi kuadhirika na ugonjwa huo baada ya kunywa maji hayo.
Pamoja na hayo, amedhibitisha kwamba wadi ya kuwachunguza walio na ugonjwa huo imetengwa huku pia akitaka uma kufika katika vituo vya afya vilivyo karibu nao iwapo wataanza kuendesha na pia kutapika.
Dkt Kipsang Marachio ambaye ni naibu mkurugeni wa huduma za kudhibiti magonjwa katika kaunti ya Baringo alisema katika muda wa miezi miwili iliyopita, visa 124 vya kipindupindu vimeripotiwa.
Marachio alisema mikakati kabambe imewekwa kuhakikisha ugonjwa huo hausambai, akiongeza kuwa wanatumai ugonjwa huo utatokomezwa hivi karibuni.
“Ugonjwa wa kipindupindu hauna mipaka. Hivyo basi tunawahimiza walio kwenye maeneo yaliyoathiriwa ya Mogotia na Marigat kudumisha hali ya juu ya usafi. Kwa sasa tumeshuhudia visa 124 vya ugonjwa huo,” alisema Dkt Marachio.
Peter Romakal kutoka kwa kitengo cha kukabiliana na majanga katika wizara ya afya alisema mikutano zaidi itafanywa ili kubuni njia ya kukabiliana na maambukizi mapya ya ugonjwa huo katika siku za usoni.