Idadi kubwa ya wanawake katika kaunti ya Mombasa, Kwale na Kilifi wanakumbwa na matatizo ya afya ya kutoweza kuzuia choo ama mkojo, kitaalamu inatambulika kuwa fistula.
Wataalamu wa afya katika kaunti hizo wamesema kwamba hali hiyo inachochewa na hatua ya wasichana kuzaa wakiwa na umri mdogo ama kushiriki mapenzi hata kabla ya kufikia umri wa kubalehe.
Mshirikishi wa shirika la Freedom of Fistula Witness Tsuma amesema takwimu zaonyesha kwamba wanawake watatu kutoka kwa kumi wanaugua maradhi hayo.
Ni kutokana na hilo, Tsuma amesema amewashirikisha madaktari kutoka kitengo cha Flying Doctor's pamoja na wale wa kaunti hizo ili kuwaokoa waathiriwa, huku akiwataka wanawake wanaogua maradhi hayo kujitokeza kwa matibabu, na kuwataka wasichana wadogo kujiepusha na mimba za mapema.
Tsuma alisema haya wakati wa huduma za kliniki Tamba zilizoandaliwa kwenye kaunti hizo siku ya Jumamosi.