Wakaazi wa lokesheni ya Mochenwa wadi ya Gesima eneo bunge la Kitutu Masaba wamewashtumu maafisa wa polisi kwa kuchukua hongo kutoka kwa wapishi pombe haramu.
Akiongea katika hafla ya mazishi siku ya Ijumaa katika sehemu ya Matunwa, chifu wa Mochenwa, Magara Makori aliwanyoshea kidole cha lawama askari wa utawala kwa kuzembea katika kazi yao.
Makori aliwalaaumu maafisa wa polisi kwa kuongezeka kwa pombe haramu katika eneo hilo.
“Mimi kama chifu wa eneo hili sitakubali kamwe kuona pombe ikiendelea kuathiri vijana wetu na wazee katika eneo hili,” alisema Makori.
Aidha, alisema yeye na manaibu wake wataanzisha msako mkali bila kuwahusisha maafisa hao wa polisi ambao utahakikisha kuwa kesi za pombe haramu zimeisha katika eneo hilo.
Makori aliwaomba wenyeji kuungana na kukashifu pombe haramu.
Kulingana na Makori pombe ambayo huuzwa katika lokesheni yake hutoka sehemu zingine kama vile kijiji cha Karantini na Kambini.
Wakati huo huo aliwatahadhalisha wanaosafirisha pombe hiyo na kuwauliza waachane na kazi hiyo kwani si halali.
Vile vile aliwaonya vijana wanaotumia madawa ya kulevya akisema kuwa watachukuliwa hatua za kisheria watakapopatikana.
Aliwaomba vijana hao kujiepusha na mambo kama hayo na kujiunga katika taasisi mbalimbali ili kuendeleza maisha yao.
“Ni wajibu wa kila mzazi kujua mtoto wake vizuri. Ni vizuri kujua kazi anayoifanya isiwe ni mmoja wanao fanya biashara haramu,” akasema Makori.