Zaidi ya visa 1,200 vya watoto walio na umri chini ya miaka 18 kubakwa vimeripotiwa katika Kaunti ya Kwale katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Akizungumza mjini Mombasa katika mkutano wa kiusalama na amani siku ya Ijumaa, Afisa Mkuu wa Polisi eneo la Matuga Patrick Oduma, alisema visa hivyo vimeongezeka kutokana na utepetevu wa wazazi katika kuwajibikia majukumu yao ya ulezi.
Oduma alisema wahudumu wa bodaboda, wazee na hata vijana wadogo wametajwa kuwa wahusika wakuu katika dhulma hizo.
Afisa huyo aliwahimiza wazazi kuviripoti visa vyote vya watoto wao kudhulumiwa katika idara husika za serikali ili washukiwa wachukuliwe hatua za kisheria.
"Tunawaomba wazazi kuwajibikia majukumu yao ya ulezi vyema ili kuzuia visa vya ubakaji katika jamii. Washukiwa lazima waripotiwe kwa maafisa wa polisi ili wachukuliwe hatua,” alisema Oduma.
Kwa upande wake, mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu eneo la Matuga, Kibibi Mwaka, amewataka wazazi kuwajibikia majukumu yao vyema, na kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata haki.