Kaunti ya Mombasa imeripotiwa kuongoza katika visa vya ubakaji wa watoto miongoni mwa Kaunti za ukanda wa Pwani kwa mujibu wa ripoti ya hivi punde iliyotolewa na Shiriki la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Alhamisi, naibu afisa mratibu wa mipangalio katika shirika hilo, Ali Fujo, alisema kuwa visa hivyo vimeongezeka hadi asilimia 53 kutoka asilimia 35 mwaka uliopita kipindi sawa na hiki.

“Tangu mwezi Januari mwaka huu, tumepokea visa vingi sana vya dhulma dhidi ya watoto katika eneo la Pwani hasa hapa Mombasa.

Kama shirika, hali hii inatutia hofu kwani waathiriwa wengi wanadhulumiwa na aidha watu wa familia au jamii yao,” alisema Fujo.

Afisa huyo aliyataja maeneo ya Jomvu, Kisauni, Likoni na Mishomoroni kama yanaongoza kwa visa hivyo kutokana na uhuni na idadi kubwa ya vijana wanaotumia dawa za mihadaratia.

Aidha, mtetezi huyo wa haki za binadamu ameilaumu idara ya usalama na vitengo vya sheria kwa kutoweka sheria kali ili kuwakabili wahusika badala ya kuwaachilia kwa dhamana kama inavyoshuhudiwa katika baadhi ya kesi.