Mhuburi mmoja Nyamira amesema kuwa hata baada ya serikali ya kitaifa kupitia kwa makamishna wa kaunti kuweka mikakati ya kuangamiza ugemaji wa pombe haramu nchini, bado ugemaji huo ungali unaendelea.
Akihitubu katika eneo la Ramba kwenye hafla ya mazishi siku ya Jumatatu, Lawrence Mokua, mhubiri wa Kanisa la Kiadventista la Ramba, alisema kuwa visa vya uuzaji wa pombe haramu vingali vinashuhudiwa katika maeneo mengi hasa katika Kaunti ya Nyamira.
Mokua alirejelea visa ambapo idadi kubwa ya watu wakimemo vijana ambao hawajahitimu umri wa kunywa pombe walipatikana wakiwa wamelewa na kulala barabani kwenye msimu wa krismasi na mkesha wa mwaka mpya.
"Ninawashtumu machifu na manaibu wao kwa kuacha ugemaji wa pombe haramu kuendelea. Wengi wao huchukua hongo kutoka kwa wagemaji ili kuruhusu biashara hiyo haramu kuendelea. Huenda hii ndio sababu tumekuwa tukishuhudia vijana wengi wakibugia pombe na kisha kulala barabarani baada ya kulewa chakari,” alisema Mokua.
Aliongeza, “Tunaitaka serikali kuu kuhakikisha kuwa mikakati imeweka yakuangamiza pombe hiyo haramu."
Mhubiri huyo aidha aliongeza kusema kuwa hatua ya Rais Kenyatta kuweka mikakati ya kuangamiza pombe haramu haijapata kufanikiwa kwa kuwa ugemaji na unywaji wa pombe haramu ungali unashuhudiwa katika maeneo mengi Nyamira.
"Tunafamu kuwa hata baada ya Rais Kenyatta kuweka mikakati ya kuangamiza pombe haramu katika maeneo mengi nchini, bado kungali watu wanaoshiriki biashara hiyo haramu. Hii ni kutokana na baadhi ya maafisa wa utawala hasa machifu na manaibu wao, kuchukua hongo kutoka kwa wagemaji ili kuruhusu biashara hiyo kuendelea," alisema Mokua.
Haya yanajiri baada ya maafisa wa polisi kule Nyamira kuwatia mbaroni zaidi ya wanafunzi 30 wenye umri wa chini ya miaka 18 kwenye maeneo ya burudani wakati wa mkesha wa mwaka mpya.