Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki amesema kuwa visa vya utovu wa usalama vimeshuka mjini Momabsa kwa sasa ikilinganishwa na miezi ya hapo awali kutokana na operesheni ya usalama inayoendelezwa na maafisa wa usalama mjini humo.
Akizungumza kwenye kikao na waandishi wa habari siku ya Jumatatu, Achoki alisema kuwa juhudi za idara ya usalama mjini humo kutokomeza uhalifi zimepiga hatua hasa katika kuyakabili makundi ya vijana ya Wakali Kwanza na Wakali Wao ambao wamekuwa wakiwahangaisha wenyeji.
“Hatutachoka. Tutaendelea kutekeleza wajibu wetu kama idara ya usalama kuhakikisha kuwa kila Mkenya anaishi bila hofu. Wachache wenye nia mbaya hawataruhusiwa kuvuruga utulivu na amani wa wengine,’’ alisema Achoki.
Hata hivyo, afisa huyo wa usalama alieleza hofu yake kuhusiana na kuongezeka kwa idadi ya vijana wanaoripotiwa kujiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya, hatua aliyotaja kama hatari kwa maendeleo na usalama mjini humo.
“Nimepata ripoti kuwa vijana wanazidi kuendela na uraibu wa mihadarati. Ukipatikana na hatia utajilaumu mwenyewe,” aliongeza Achoki.
Kamishna huyo vilevile alisema kuwa idara ya usalama imetoa ahadi kwa vijana ambao walijiunga na makundi haramu ikiwemo lile la al-Shabaab, kuwa watasamehewa iwapo watajisalimisha kwa serikali.