Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa Mombasa Hassan Joho amesema kuwa masaibu yanayokumba biashara zake za kusafirisha mizigo kupitia Bandari ya Mombasa yalianza alipojihusisha na maswala ya kisisasa.

Gavana huyo alisema wale wanaodai kuwa anaendesha biashara zisizo halali bandarini ni watu wenye nia ya kumkandamiza baada ya kuona kwamba biashara zake zinaendelea kunawiri.

Akizungumza katika mahojiano kwenye runinga ya Citizen siku ya Jumanne, Joho alisema kuwa alianza kudaiwa kuendeleza biashara ya dawa za kulevya tangu alipokuwa mbunge wa Kisauni.

“Nilianza kuambiwa kuwa nafanya ulanguzi wa dawa za kulevya punde tu nilipochagulia kama mbunge wa Kisauni mwaka wa 2009,” alisema Joho.

Wakati huo huo, Joho alisema kuwa Kenya imekuwa na tamaduni potovu ambapo mtu hupigwa vita pindi anapoanza kunawiri kibiashara.

Alikashifu tabia hiyo huku akidai kwamba hali hiyo inarudisha nyuma maendeleo na kuwafanya wafanyibiashara kushindwa kujiendeleza.

“Inasikitisha kuona kwamba hapa Kenya ukianza kunawiri kimaisha utaona watu wakianza kutafuta sababu za kukukandamiza na hasa viongozi wa kisiasa ndio walengwa wakuu,” alisema Joho.

Matamshi yake yanajiri huku mahakama kuu mjini Mombasa ikitarajiwa kusikiliza ombi la mamlaka ya KRA la kutaka mabohari yanayohusishwa na familia ya gavana huyo kuendelea kufungwa.

Mabohari hayo yalifungwa wiki mbili zilizopita ili kurahisisha uchunguzi baada ya madai kuibuka kwamba yanaingiza bidhaa ghushi pamoja na kukwepa kulipa kodi.