Matamshi ya Mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire kumtaka mpinzani wake Shadrack Mose kuwania cheo cha spika wa bunge la kaunti ya Nyamira yameibua joto kali la kisiasa baina ya viongozi hao wawili.
Akihutubia waombolezaji kwenye hafla ya mazishi katika kijiji cha Nyabuya kule Gesima, Mose aliyataja matamshi ya mbunge huyo kama yasiyo na maana na kumdhalilisha, huku akiahidi kumpa upinzani mkali mbunge huyo kwenye uchaguzi mkuu ujao.
"Kwa kweli Mungu hujibu maombi ya watu wake na mtakubaliana nami kuwa kuna mtu ameshindwa kuifanya kazi yake, na sijamwambia Bosire anitafutie kazi ya kuwa spika wa bunge la kaunti ya Nyamira kwa kuwa nia yangu ni kuwafanyia kazi wananchi wa Kitutu Masaba," alisema Mose.
Mose aidha alimtaka Bosire kuwafanyia wakazi wa eneo bunge hilo kwa usawa bila kujali iwapo walimpigia kura au la.
"Mimi sio mwanachama wa ODM, lakini namshauri awafanyie watu wote wa Kitutu Masaba kazi iwe walimpigia kura au la," alisema Mose.
Bosire alinukuliwa siku ya Jumapili akisema kwenye hafla ya kuchangisha pesa kule Machuririati kuwa Mose anafaa kuwania kiti cha spika wa bunge la kaunti ya Nyamira badala ya kuwania kiti cha ubunge cha eneo la Kitutu Masaba.