Viwango vya maambukizi ya ukimwi miongoni mwa waraibu wa mihadarati wanaotumia sindano vimeripotiwa kupungua kwa kiwango kikubwa katika maeneo ya kusini mwa Pwani, hasa eneo la Ukunda.
Kulingana na ripoti ya hivi punde, haya yametokana na hatua ya waraibu hao kutumia sindano safi kila mara wanapozihitaji, kinyume na hapo awali ambapo sindano moja ingetumika kwa zaidi ya waraibu 10.
Kwenye mahojiano na waandishi wa habari katika eneo la Ukunda siku ya Jumatatu, Saria Salim, afisa kutoka kituo cha kurekebishia tabia cha Teenswatch, alisema hali hiyo imesaidia kupunguza visa vya waraibu hao kuambukizwa magonjwa mengine kupitia kujidunga na sindano ikilinganishwa na miaka ya awali.
“Kwa sasa kutokana na uchunguzi tuliofanya, tumebaini kuwa visa vya waraibu kujiambukiza ukimwi kwa kutumia sindano vimepungua. Hali hiyo inatokana na wao kutumia sindano mpya kila wakati wanapojidunga,” alisema Salim.
Aidha, afisa huyo alifichua kuwa kituo hicho kimeweka mikakati kabambe inayolenga kuwasaidia waraibu walioasi matumizi ya dawa za kulevya kurejelea hali yao ya kawaida.