Vyama 17 vya akina mama kutoka wadi ya Gachuba eneo bunge la Kitutu masaba kaunti ya Nyamira wako na sababu ya kutabasamu baada ya kufadhiliwa mbolea na mbegu ya mboga kutoka kwa mwanasiasa wa eneo bunge hilo Victor Swanya Ogeto.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanasiasa huyo kutoka eneo bunge la Kitutu Masaba alifadhili akina mama hao mbegu ya mboga kama managu,saga kabegi na mbolea,  siku ya ijumaa katika shule ya msingi ya Bonyunyu iliyoko eneo bunge la Kitutu Masaba ili kujiimarisha kiuchumi na kibiashara.

Aidha aliwaomba akina mama hao kuweka bidii kwa kilimo na kujiendeleza kibiashara huku akiwaomba akina mama wengine ambao hawajajiunga kwa chama chochote kufanya hivyo ili kujiendeleza kibiashara.

“Huu mradi nimeanzisha utawasidia akina mama na nimeanzia wadi ya Gachuba na tutaenda sehemu zote zilizoko eneo bunge hili la Kitutu Masaba ili akina mama wapate kujiendeleza,”alisema Ogeto.

Aliongezea, “Hatutaendelea kama hakuna miradi katika sehemu hii. Tutawafundisha akina mama hawa jinsi ya kupanda mboga na wakati wamevuna tutawafundisha pia jinsi ya kuweka mboga hizo ili zisiharibike.”

Aidha mwanasiasa huyo aliwaomba viongozi wote kushirikiana pamoja kuendeleza vyama vyote vilivyoko katika eneo bunge hilo na kuomba serikali ya kaunti ya Nyamira kuwatafutia akina mama hao soko la mboga zao.