Vyama vya kutetea maslahi ya waalimu vya KNUT na KUPPET vimetakiwa kuungana ili kujipa nguvu zaidi ya kukabiliana na serikali katika juhudi zao za kupigania maslahi ya waalimu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la NAHURINET, David Kuria, alivitaka vyama hivyo viwili kutupilia mbali tofauti zao na kuungana kwa manufaa ya mwalimu wa Kenya.

Akiongea siku ya jumapili katika mtaa wa Kivumbini wakati wa hafla ya kuzindua ujenzi wa shule moja inayodhaminiwa na shirika hilo, Kuria alisema kuwa vyama vya KUPPET na KNUT vina lengo moja la kuboresha maslahi ya waalimu na kushangaa ni kwa nini haviwezi kufanya kazi kama chama kimoja.

“KUPPET na KNUT wamekuwa na tofauti kwa muda mrefu na hizo tofauti zimechangia katika kufeli kwao katika kutetea waalimu.Iwapo wangeungana na kuwa chama kimoja basi ingekuwa rahisi kwao kuafikia lenog lao. Ingekuwa rahisi kwao kukabiliana na serikali iwapo wangeungana na kuwa kitu kimoja na kuongea kwa sauti moja,” alisema Kuria.

Kuria vilevile aliwataka viongozi wa KNUT na KUPPET kuweka maslahi ya waalimu mbele ya maslahi yao ya kibinafsi.

“Ni jambo la wazi kwamba viongozi wa KNUT na KUPPET wanatumia nyadhifa zao na shida za waalimu kujitafutia makuu na hadi pale watakapo weka maslahi ya waalimu mbele ndipo shida zinazowakumba waalimu zitakapotatuliwa,” alisema.

Alitoa wito kwa waalimu kote nchini kufunza wanafunzi kwa roho moja wanaporudi shuleni baada ya mgomo wa majuma mawili huku akiwataka kuwa na imani kwa mahakama ya kiviwanda kuwapa suluhu la kudumu kwa matatizo yanayowakumba.