Baraza la kushughulikia maslahi ya wanahabari Juma nne liliandaa kongamano maalum mjini Eldoret la kujadili maswala tofauti katika sekta ya uanahabari.
Kongamano hilo lililojumuisha wanahabari kutoka vituo mbalimbali katika kaunti ya Uasin Gishu, wanafunzi wanaosomea uanahabari na wananchi kwa jumla, lilifanyika katika mkahawa wa Comfy.
Kati ya maswala yaliyojadiliwa ni jinsi ya kudumisha ukweli na uadilifu baina ya waandishi wa habari.
Akizungumza katika kongamano hilo mkurugenzi mkuu wa baraza hilo, Haron Mwangi, alitoa wito kwa vyumba vyote vya habari kuzingatia uwezo wa kitaaluma wanapowaajiri wafanyikazi katika vituo vyao.
Aidha umma umehimizwa kujiepusha na matamshi yatakayochochea chuki wakati wanapotoa michango yao katika vipindi vya redio na televisheni na kudumisha amani na umoja kwani sisi sote ni familia moja.
Baraza hilo lilizinduliwa mwaka 2007 ili kudhibiti maswala ya utangazaji na kuimarisha maadili mema baina ya wanahabari.