Vyombo vya habari vimeombwa kuwapa mafunzo wananchi kuhusu hatari za mvua nzito ya EL Nino inayotarajiwa kuanza kunyesha mwezi wa Oktoba hadi Desemba.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi mkuu wa Idara ya hali ya anga katika Kaunti ya Kisii Henry Sese, ambaye alisema mafunzo kwa wananchi ni muhimu ili kuepukana na hatari hizo za mvua.
Kulingana naye, idadi ya watu wengi mkoani Nyanza hawabaini hatari za mvua hiyo, huku vyombo vya habari vikiombwa kujaribu kila wawezalo ili kuwapa mafuzo wananchi kuhusu mvua hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Alhamisi mjiniKisii, Sese alisema mvua hiyo ina madhara mengi kwa wananchi wasipokuwa na mafunzo hususan.
“Wengi wa wananchi wa kaunti ya Kisii hata mkoani Nyanza hawajui hatari za EL Nino. Mvua hii inayokuja wananchi hawastahili kulima kwenye mabwawa, kujikinga kwa miti wakati inaponyesha na mengine mengi,” alisema Sese.
Wakati huo huo, mkurugenzi huyo aliomba serikali ya kaunti ya Kisii kukarabati baadhi ya barabara ambazo ni mbaya ili wakati wa mvua unapowadia barabara zipatikane tayari zimekarabatiwa.
“Naomba serikali yetu ya kaunti kukarabati barabara na chochote kitokeacho serikali iwe tayari kutoa usaidizi kwani mvua hii inayotarajiwa ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini,” aliongeza Sese.
Aidha, alisema miongoni mwa magonjwa ambayo huenda yakaathiri wananchi ni Malaria, Kipindupindu miongoni mwa mengine.