Baadhi ya wabunge wa jimbo la Nakuru wameitaka serikali kuu kugatua hazina ya kitaifa kwa walemavu ili huduma hiyo isimamiwe na serikali za kaunti na kuhakikisha watu wenye ulemavu wamehudumiwa ipasavyo.
Wakiongozwa na mwakilishi wa Wadi ya Turi Michael Wang’ombe, Florence Njoroge (Elburgon) na Agnes Chelotich (Marioshoni ), viongozi hao wamesema shirika hilo husajili walemavu kupitia makao yake makuu jijini Nairobi, jambo ambalo limesababisha walemavu wengi kukosa kunufaika na vifaa vinavyotolewa na serikali kupitia idara hiyo.
Wakiongea kwenye hafla ya kutoa vifaa kwa watu wenye ulemavu mjini Molo, waakilishi hao wamesema licha ya serikali kuwekeza kima cha Shillling milliioni 100 kwa lengo la kuimarisha maisha ya wananchi wenye ulemavu, bado ufadhili huo haujafika mashinani .
Naibu msimamizi wa hazina hiyo Bernard Aduda amesema hazina hiyo imetoa ufadhili wa vifaa vya zaidi ya milioni 1.5 ili kufaidi walemavu wilayani Molo na Kuresoi.
Amesema wilayani Kuresoi, watu 36 wamenufaika na mgao wa bidhaa hizo ikiwemo vyombo vya ukulima, mashine za ususi, vyombo vya seremala, Cherehani, vigari vya magurudumu miongoni mwa bidhaa zingine zenye thamani ya Shillingi720,000.
Aduda ameongeza kuwa wilayani Molo vyombo vya thamani ya Shillingi 850,000 zimekabidhiwa walemavu huku walionufaika wakielezea matumaini yao kwamba vyombo hivyo vitawasaidia kufungua biashara na kujikimu katika mustakabali wao.
Ameuliza wazazi wenye watoto walemavu kutowatelekeza kwa kuwanyima haki za kimsingi, akisema watoto hao huenda wana vipawa adimu ambavyo vikipigwa msasa vitapelekea wenye ulemavu kutumikia jamii.