Waalimu katika eneo la Gucha kaunti ya Kisii wameelezea masikitiko yao kutokakana na kuongezeka kwa vifo vya kutatanisha vya waalimu sehemu hiyo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

 Wakiongozwa na katibu mkuu wa chama cha waalimu nchini KNUT tawi la Gucha, Sam Nyairo, waalimu hao walisema kuwa kwa majuma mawili eneo hilo limekuwa likishuhudia mauaji ya waalimu ambayo msingi wake haujulikani.

 “Ni jambo la kusikitisha sana kuona walimu wakiuawa kinyama na serikali haichukui hatua yo yote,” akasema Nyairo.

Nyairo alilaumu wanausalama kwa kujikokota kuwatia mbaroni washukiwa hata baada ya ripoti kupigwa katika vituo vya polisi.

Kwa sasa eneo hilo limeshuhudia vifo vya waalimu wanne kwa kipindi cha majuma mawili yaliyopita. Waalimu hao wameuawa kwa njia ya kutatanisha.

Jambo hili limewaogofya wakaazi huku wakiiomba serikali ichukue hatua kuzuilia maafa kama haya.

 Kisa cha hivi karibuni kikiwa ni mauaji ya naibu wa mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Egetuki, Joseph Nyatundo, ambaye aliuawa na mwili wake kutupwa kando ya barabara.

Marehemu Nyatundo, baba wa watoto watano, anadaiwa kutoka shuleni Jumatatu jioni alipofunga kazi yake lakini hakufika nyumbani kwake.

Mwili wake ulipatikana asubuhi ya siku iliyofuatia kando mwa barbara inadaiwa kuwa wapita njia waliijulisha familia yake.

Mwenyekiti wa KNUT tawi la Gucha, Stephen Otundo, amewanyoshea kidole cha lawama walinda usalaama kwa kutochukua hatua tangu visa vya kuwadhurumu waalimu vianze.

 Kamanda wa polisi kaunti ya Kisii Simon Kiragu amesema kuwa washukiwa watano wametiwa mbaroni na wanawasaidia wapelelezi na uchunguzi.