Idara ya elimu katika kaunti ndogo ya Rongai inaendeleza uchunguzi dhidi ya shule ambazo zinaendelea kuzuilia vyeti vya wanafunzi waliokamilisha kidato cha nne kutokana na ukosefu wa kumaliza kulipa karo.
AkizungumzaJumatano, mkuu wa idara ya elimu katika kaunti ndogo ya Rongai George Ngao alisema kuwa amekuwa akipokea malalamishi kutoka kwa wanafunzi na wazazi dhidi ya swala hilo.
Alisema kuwa serikali ilikuwa imeahidi kuwa itawalipia wanafunzi hao baki ya karo ambayo ilikuwa imebakia na jukumu la wakuu wa shule kuwapa wanafunzi hao vyeti hivyo.
“Sioni ni sababu gani mwalimu mkuu akose kufuata sheria ambayo inatolewa na serikali, ikiwa serikali kupitia naibu wa rais ilisema wanafunzi hao wapewe vyeti vyao, sioni sababu ya kuzuiliwa,” Ngao alisema.
Aliongeza kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakikosa kazi wanapoenda kuzitafuta, kutokana na kuzuiliwa kwa vyeti vyao.
Alisema kuwa uchunguzi utakapokamilika atahahakisha walimu ambao watapatikana na hatia ya kuzuilia vyeti vya wanafunzi watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Itazingatiwa kuwa mwaka wa 2014, naibu wa rais William Ruto alikuwa ameagiza walimu wakuu kuwapa wanafunzi ambao hawajakamilisha karo vyeti vyao kwani serikali itakamilisha karo zao.