Wafanyibiashara wa kuuza simu na bidhaa za kielektroniki katika eneo la Kisauni wamelalamikia usalama wa biashara zao wakisema huenda ikawalazimu kufunga biashara hiyo mapema kufuatia uporwaji wa simu na bidhaa nyengine za kielektroni mchana mweupe na waathiriwa wa dawa za kulevya almaarufu Mateja.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na Esther Muasya anayemiliki duka hilo katika eneo la Mtopanga, mateja hujifanya kuwa wateja wanaohitaji kununua simu kisha baadae hurudi na kuiba mali hiyo baada ya kujua aina ya simu wanayoitaka. 

Esther pia ameongeza kuwa wengi wa mateja huwa sio nia yao bali hutumwa na watu wenye akili timamu kwenda kuiba ili kuwauzia kwa bei rahisi.

Aidha, anasema kuwa kwa sasa imekuwa desturi kwa waathiriwa wa dawa za kulevya kuzurura kwenye maeneo ya maduka hayo hususani wakati wa mchana kisha baadae ifikapo mwendo wa saa kumi na mbili jioni huanza kutekeleza uovu huo aidha kwa kuwatisha na visu ama kupora kwa kutumia nguvu.

Wahudumu hao wanasema kuwa mateja hao ni wakazi wa maeneo hayo na ni vigumu kutabiri njia wanazotumia kufika katika maduka ya simu.

Hata hivyo wameitaka idara ya usalama kaunti ya Mombasa kuingilia kati na kuwapeleka maafisa wa polisi eneo hilo ili kuimarisha hali ya usalama eneo hilo kwani kwa sasa inawalazimu kufunga biashara zao mapema kutokana na kukithiri kwa utuvo wa usalama.

Image caption, mhudumu wa duka la kuuza simu, wahudumu wamelalakia wizi wa simu katika eneo la Kisauni.