Waathiriwa wa ugonjwa wa kipindupindu mjini Naivasha wamefikia 20 huku ikihofiwa kuwa watu zaidi huenda wakaugua ugonjwa huo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Ugonjwa huo uliripotiwa kuanzia wiki jana baada ya watu watano kufikishwa kwenye hospitali ya kaunti ndogo ya Naivasha.

Kulingana na afisa mmoja wa afya kwenye hospitali hiyo ya Naivasha, idadi ya wagonjwa imepanda kutokana na maji chafu kwenye mtaa duni wa Kihoto.

“Wote hao ni kutoka mtaa duni wa Kihoto ambapo wafanyikazi wa mashamba ya maua wanatumia maji chafu,” mhudumu huyo wa afya alisema.

Daktari Samuel Mwaura wa kaunti ya Nakuru alisema tayari wametuma maafisa wa afya kwenye eneo hilo ili kukabiliana na hali. Kihoto kuna familia nyingi ambazo huishi katika mazingira mabaya kutokana na umaskini.