Vijana walioathirika na utumizi wa dawa za kulevya katika Kaunti ya Mombasa wamelalamikia kudhulumiwa na maafisa wa polisi wanapotiwa nguvuni.
Waathiriwa hao wa mihadarati wamewataka maafisa wa polisi kutowanyanyasa.
Wamependekeza kuidhinishwa mikakati mwafaka ya kuwasaidia, badala ya polisi kuwapiga na kuwadhulumu.
Wakiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, wakiongozwa na Maimuna Bakari, waathiriwa hao walisema kuwa itakuwa vyema iwapo watapelekwa katika vituo vya kurekebisha tabia na kupata tiba maalum itakayowasaidia kujinasua kutoka jinamizi hilo.
"Sisi tunawalaumu maafisa wa polisi na jinsi wanavyotudhulumu pindi wanapotutia mbaroni. Badala ya kutupeleka hospitali wanatupiga na kutunyanyasa ilhali sisi tunatarajia hao ndio watusaidie,” alisema Maimuna.
Wakati huo huo, wamependekeza waathiriwa wengine wa utumizi wa mihadarati kujitokeza ili kupata matibabu.
Aidha, wameyashinikiza mashirika mbalimbali pamoja na Idara husika kuwasaidia kupata tiba ili waweze kujikimu mashinani.