Wananchi na viongozi mbalimbali mjini Mombasa waliungana Jumapili katika kanisa la Joy In Jesus Likoni kwa ibada maalum miaka miwili baada ya kanisa hilo kushambuliwa na magaidi.
Miongoni mwa walioudhuria ibada hiyo ni waathiriwa wa shambulizi hilo walionusurika baada ya kupata majeraha ya risas. Baadhi yao sasa ni walemavu.
Waathiriwa hao walielezea jinsi maisha yao yalivyobadilika miaka miwili baadaye na jinsi wamekuwa wakipitia hali ngumu za kifamilia.
Diana Maloba alifanyiwa upasuaji mara 11 kutokana na majeraha ya risasi. Alisema alitengana na mumewe kutokana na gharama kubwa ya matibabu.
Wakati huo huo Diana alisema kuwa kumbukumbu za shambulizi hilo bado zipo licha ya kuwa ni muda mrefu umepita kufikia sasa.
“Mimi sikujua wakiingia, nilijipata nimepigwa risasi niko chini na sikujielewa kuanzia hapo, ilikuwa siku mbaya sana kwangu,” alieleza Diana.
Katika shambulizi hilo lililotokea mwezi Machi mwaka 2014, watu wanne walifariki na zaidi ya watu 15 wakijeruhiwa.
Wengine waliohudhuria ibada hiyo ya Jumapili ni mbunge wa eneo hilo la Likoni Masoud Mwahima pamoja na kamishna wa kaunti ya Mombasa Evan Achoki.