Akina mama waliojifungua baada ya wao kubakwa wakati wa ghasia za uchaguzi mkuu wa 2007/2008, wanahangaishwa wanapowatafutia watoto hao vyeti vya kuzaliwa.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakizungumza siku ya Alhamisi, ambapo nchi ya Kenya iliungana na ulimwengu kuadhimisha siku ya kimataifa kuhusu haki, waathiriwa hao waliiomba serikali kutekeleza kikamilifu ripoti iliyotolewa na tume ya ukweli, haki na maridhiano (TJRC) ili wapate haki.

‘‘Tunaiomba serikali itusaidie tupate haki sisi waathiriwa wa vita vya baada ya uchaguzi. Tumeteseka sana na tunataka tupate haki kama wakenya,’’ alisema mmoja wa waathiriwa hao.

Jacquiline Mutere, kutoka Shirika la Grace Ajenda, linalowapa hifadhi zaidi ya akina mama 150, alisema wanaitishwa stakabadhi za wazazi wa kiume ilhali walibakwa na watu wasiojulikana.

‘‘Watoto hawajapata vyeti vya kuzaliwa kwa sababu mama zao wanaagizwa majina ya baba zao wanapoenda kutafuta vyeti hivyo ilhali wanawake hawa hawajui majina ya watu waliowabaka,’’ alisema Mutere.

‘‘Shida nyingine ni kwamba cheti za kuzaliwa huagizwa hadi shuleni na hata mtu anapotafuta kipenda anapotimu umri wa miaka 18. Kwa hivyo, itakuwa vigumu zaidi kwa watoto hawa kupata fursa kama hizi,’’ aliongeza Mutere.

Mutere pia alisisitiza kuwa ni vyema iwapo serikali kuu itaungana na wadau husika ili watafute mbinu ya kuwasaidia waathiriwa wa vita hivyo kupata haki.

Aidha serikali imesema kuwa iko mbioni kuhakikisha kuwa ripoti ya haki, ukweli na maridhiano imetekelezwa kikamilifu ili waathiriwa hao wapate haki ikizingatiwa kuwa ripoti hiyo ni ya matumaini makubwa kwao.