Msimamizi na mhudumu wa kitengo cha kuwahudumia waathiriwa wa visa vya unyanyasaji wa kijinsia katika Hospitali Kuu ya Mkoa wa Bonde la Ufa iliyoko Nakuru amewataka waadhiriwa wa dhulma hizo kuripoti visa hivyo hospitalini.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika mahojiano na mwandishi huyu, msimamizi huyo Teophila Murage, alisema kwa kufanya hivyo, waathiriwa wa ubakaji na visa vya ulawiti wanaweza kufaidika pakubwa kwa kupata usaidizi endapo watapata magonjwa kutokana na matukio hayo.
“Kwa wakati mwingine, labda utataka haki itendeke, na kuna mambo ambayo tunaweza kuzuia endapo utafika hospitalini haraka iwezekanavyo. Tunaweza kuzuia magonjwa kama vile virusi vya ukimwi kama hauna virusi hivyo na pia tunaweza kuzia magonjwa kama Hepatitis B,” alisema Bi Murage.
Murage alisema kuwa zaidi ya visa mia moja vya dhuluma za kijinsia huripotiwa kila mwezi katika hospitali hiyo akiongeza kuwa visa vingi ambavyo huripotiwa ni vya watu walio na umri ulio kati ya miaka 14 na 17.
Mhadhiri wa masuala ya ushauri na saikolojia katika Chuo kikuu cha St Paul tawi la Nakuru alisema kuwa visa vingi vya dhulma za kijinsia vinaashiria ukosefu wa ushauri bora na mfano mwema miongoni mwa wazazi, walimu, wadau muhimu pamoja na mazingira yasiyofaa.
Isitoshe, alitaja ukosefu wa mawasiliano ya wazi na yafaayo baina ya wazazi na watoto wao kama changamoto inayokabili jitihada za kutatua swala hili.