Wanaume wawili wameokolewa katika mtaa wa Mabanda wa Kasuitu, mjini Athi River, ambako walikuwa wamekwama kwa zaidi ya saa 12 kutokana na mafuriko.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Richard Musyoki (21) na Joshua Kimathi (18) walilazimika kulala usiku mzima katika nyumba yao ya mabati iliyokuwa imefurika kabla ya kuokolewa siku ya Jumamosi.

Akizungumza katika eneo la tukio hilo, Naibu Kamishna wa Athi River David Tegutwa alisema kuwa wawili hao ambao ni wafanyakazi katika shamba moja mtaani humo, walikuwa wamelala katika nyumba hiyo waliojengewa na mwajiri wao, Mto Athi ulipovunja kingo zake siku ya Ijumaa na kusababisha mafuriko.

Tegutwa alisema waathiriwa hao walionekana na wanawake waliokuwa wakivuna mboga baada ya kupiga kamsa.

Naibu kamishna huyo alisema kuwa wanawake hao waliwafahamisha polisi jamii wa eneo hilo kuhusu tukio hilo, nao wakapiga ripoti kwa afisi yake.

Aliongeza kuwa alifika katika eneo hilo akiwa ameandamana na maafisa wa polisi kutoka kaunti ndogo ya Mavoko, pamoja na maafisa wa zima moto waliofanikisha zoezi hilo la kuwaokoa wanaume hao kwa kushirikiana na wakaazi.

"Wanaume hao wana bahati sana kwa sababu walionekana mapema kabla ya hali hiyo kuwa mbaya zaidi. Nilipokea ripoti kupitia njia ya simu leo asubuhi na kupanga timu ya waokoaji kwa haraka, hatua iliyotuwezesha kuwaokoa wanaume hao,” alisema Tegutwa.

Tegutwa alisema kuwa waathiriwa hao walikuwa wamekaidi amri kutoka kwa mamlaka mbalimbali ya kuwataka kuhamia maeneo ya juu msimu huu wa mvua.

Aliongeza kuwa serikali ya kitaifa pamoja na ile ya kaunti ya Machakos zilikuwa zimewatahadharisha wanaoishi katika maeneo ya hatari yaliyoko karibu na Mto Athi na Mto wa Mawe kuhamia maeneo salama wakati huu ambapo mvua kubwa inaendelea kushuhudiwa nchini.

Aidha, alisema kuwa kwa vile wawili hao walipuuzilia mbali tahadhari hizo, huenda wakashtakiwa kwa kujaribu kujitoa uhai.

Bwana Tegutwa alisema kuwa Mto Athi na mto wa Mawe zilifurika kufuatia mvua kubwa inayoshuhudiwa katika maeneo ya Ngong katika kaunti za Kajiado na Nairobi.

Alisema kuwa Kwa Mang'eli, Jam City Kasuitu, Kaanani mjini Athi River pamoja na Kasuitu na Mto Wa Mawe ni baadhi ya madaraja yaliyofurika kutokana na mvua kubwa.

Mwandishi huyu aliweza kudhibitisha kuwa daraja lililoko katika barabara ya Namanga pia lilikuwa imeathirika na mafuriko hayo.

Tegutwa alionya kuwa watakaokaidi maagizo ya kuhama kutoka maeneo hatari watachukiliwa hatua za kisheria.