Wabunge wa Pwani wanaounga mkono mrengo wa Jubilee wanapanga kuunda chama kimoja watakachotumia katika uchaguzi wa 2017 ili kuhakikisha kuwa wanajumuishwa serikalini.
Wakiongozwa na mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga na Ganze Peter Shehe, wabunge hao wanadai njia ya pekee itakayosaidia mkoa wa Pwani kuwa ndani ya serikali ijayo ni kuwa chini ya mwavuli mmoja na kuzungumza lugha moja.
Wakizungumza katika mikutano miwili tofauti katika maeneo ya Mariakani na Marere mwishoni mwa juma, watunga sheria hao walisema mkoa wa Pwani umekuwa ukitengwa wakati wa uteuzi wa nyadhifa mbali mbali serikalini licha ya wao kuunga mkono serikali ya Jubilee.
''Wapwani tumesazwa sana katika uongozi nchini, wakati umefika sasa tuje pamoja, tuzungumze lugha moja ili tupata nguvu ya kupigania nafasi yetu katika serikali," alisema Gunga.
Wabunge hao walitoa mfano namna vyama vya TNA na URP vilivyofaidi katika uteuzi wa baraza la mawaziri uliofanywa na Rais Uhuru Kenyatta mwezi wa Novemba kutokana na muungano wao chini ya mrengo wa Jubilee.