Wabunge kutoka Mombasa wametakiwa kutoa mwelekeo kwa serikali ya Kaunti ya Mombasa na wala sio kusifu na kuwapotosha wakaazi wa kaunti hiyo kwa kila kitu ambacho serikali hiyo inatekeleza.
Akiongea baada ya kuhudhuria misa katika kanisa moja jijini Mombasa siku ya Jumapili, Mbunge wa Nyali Hezron Awiti alitoa madai kuwa huenda kuna wabunge walikuwa wakishirikiana na Gavana Hassan Joho katika kutekeleza miradi ya kibinafsi na hivyo hawawezi mkosoa panapo takikana.
Awiti alisema kuwa kati ya wabunge sita wa Kaunti ya Mombasa, ni yeye tu na Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima ambao wamekuwa wakimkosoa gavana huyo huku wote waliobaki wakionekana kumsifu hata wakati ambapo anakosea.