Seneta mteule wa Kaunti ya Mombasa amesema kuwa wabunge waliovuruga hotuba ya rais katika bunge la kitaifa juma lililopita wanapaswa kuadhibiwa na kisha kushauriwa kuhusu umuhimu wa majukumu yao na jinsi wanavyopaswa kujiheshimu kama Viongozi.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Seneta Emma Mbura alisema kwamba ni kinyume na maadili ya kiongozi yeyote kuvuruga hotuba iliyolenga kuangazia maswala muhimu yanayotekelezwa na rais.
Seneta huyo alisema kwamba ni lazima hatua zifaazo dhidi ya wabunge hao zichukuliwe.
Aidha, Mbura alisema kwamba ni lazima wabunge wabadli mienendo yao na kujiheshimu wao wenyewe sambamba na kuheshimu afisi wanazohudumu na kukoma kupotoka kimaadili mbele ya umma.
Seneta huyo aliwapongeza wabunge wa eneo la Pwani kwa kukosa kushirikiana na wenzao wa ODM katika kumkosoa na kumpigia filimbi Rais Uhuru Kenyatta wakati alipokuwa akilihutubia taifa.
“Tunataka sheria ichukue mkondo wake kwa kuwaadhibu wabunge waliokosa heshima bungeni na kumzomea rais alipokuwa akitoa hotuba yake kwa Wakenya,” alisema Mbura.