Siku tatu tu baada ya kukamilika kwa kongamano la baraza la magavana nchini, wabunge wa kitaifa wa kaunti ya Kwale wamemkashifu gavana wa Kwale Salim Mvurya kwa madai ya kutumia shilingi milioni 27 za serikali hiyo katika shughuli za kuendeleza kongamano la tatu la magavana huko Meru.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakiwahutubia wahanga wa kimbunga huko Kinondo katika eneo bunge la Msambweni, viongozi hao mbunge wa LungaLunga Khatib Mwashetani na mwakilishi wa wanawake Kwale Zainab Chidzuga wamesema haiamkiniki kwa serikali hiyo kutumia kiasi kikubwa cha fedha katika kufadhili shughuli za baraza hilo wakati wakaazi wa kaunti hiyo wanakumbwa na mafuriko na wengine kukosa makao baada ya makaazi yao kusombwa na kimbunga.

Kwa upande wake Zainab Chidzuga mwakilishi wa wanawake Kwale, amemtaka gavana Mvurya kuwajibika na kuelezea wananchi namna serikali yake ilivyoafikia hatua ya kutoa kiasi hicho cha fedha na jinsi ilivyotumia fedha hizo.

Hata hivyo gavana wa Kwale Salim Mvurya amewasuta vikali viongozi hao na kuwataka wafanye wajibu wao kama wabunge badala ya kuingilia kazi za serikali hiyo.