Mwanasiasa kutoka eneo bunge la Nyaribari Chache Kaunti ya Kisii amewakosoa wabunge wa bunge la kitaifa nchini kwa kupitisha miswada ya elimu bila kuwahusisha washikadau wote wa elimu.
Rael Otundo alisema ikiwa wabunge wanahitaji kufanya jambo fulani, wanastahili kuhusisha pande husika ili kukomesha shida kutokea baada ya kupitisha mswada.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Kisii, mwanasiasa huyo aliomba wabunge wote nchini kuwahusisha washikadau husika kabla ya kupitisha miswada huku akitumia mfano wa kupitisha mswada wa kuondoa utumizi wa viboko shuleni jambo ambalo alisema limechangia wanafunzi kukosa heshima na hata kuanguka mtihani wa kitaifa.
“Naomba wabunge wawe na heshima na kuwahusisha washikadau husika hasa katika sekta ya elimu kabla ya kupitisha mswada dhidi ya sekta hiyo,” alisema Otundo.
Aliongeza: “Huwa shida inatokea kwa kutohusisha pande zote za washikadau. Hatutakubali hilo kuendelea kufanyika nchini na kuanzia sasa, naomba wabunge wawe wanafuatilia mkondo ufaao wanapofanya jambo linalowahusu wakenya wa kawaida.”
Mwanasiasa huyo alisema wizara ya elimu inastahili kufanya mambo kwa kuhusisha washikadau wote na kukosoa wizara hiyo kwa kuondoa mtihani wa mwigo katika shule za humu nchini kwa kusema itakuwa vigumu kujua ikiwa wanafunzi wamejitayarisha ipasavyo kwa mtihani wa kitaifa.