Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya polisi iliandaa zoezi la kuwasajili makurutu wapatao 10,000 siku ya Jumatatu kote nchini.

Katika kaunti ya Kisumu, idadi ya wenyeji waliofika kwenye vituo mbali mbali vya kujisajili ilikuwa chini mno.

Kata ndogo ya mashariki mwa jiji la Kisumu ni mojawapo ya maeneo ambayo idadi ya wakaazi waliojitokeza kusajiliwa kujiunga na polisi ilikuwa ndogo mno kinyume na matarajio.

Akizungumza na wanahabari wakati wa zoezi hilo jijini Kisumu, kamanda wa polisi wa utawala katika Kaunti ya Kisumu Joseph Keitany, alisema kuwa idadi ya wakaazi waliojitokeza haikuwa ya kuridhisha mno, huku wengi wao wakiwasili katika vituo hivyo wakiwa wamechelewa.

“Tumekubaliana kwamba waliofika kwa kuchelewa baada ya kupata kuchanganyikiwa na mahala maalum kunakotekelezwa usajili huo, wataruhusiwa kushiriki katika zoezi hilo. Kukamilika kwa zoezi hili ni saa kumi na moja jioni,” alisema Keitany.

Wakati huo huo, wakaazi waliojitokeza walilalamikia ukosefu wa habari kuhusiana na maeneo ya usajili, hali waliyosema iliwachanganya na kusababisha wao kufika katika vituo hivyo wakiwa wamechelewa.

“Nilipofika stadium nilipata hakuna mtu. Hapo hapo nikafululiza hadi Kituo cha polisi cha Central, nikatumwa hadi shule ya Lions Kisumu. Nilipofika huko pia hakukuwa na yeyote, nikaambiwa niende hadi Mamboleo. Hivyo ndivyo nilivyopoteza muda na kukosa kushiriki katika zoezi hilo,” alisema mwanadada mmoja aliyejitokeza kushiriki zoezi hilo.

Wakaazi hao wameitaka idara ya polisi kuhakikisha kuwa ujumbe kuhusu vituo vya usajili wa makurutu vinawafikia wananchi kwa wakati ufao katika siku za usoni.