Idara ya mazingira katika kaunti ndogo ya Rongai, imetoa onyo kwa wafanyibiashara wanaotupa takataka katika barabara ya kutoka eneo la Mercy Njeri mjini-Nakuru na ile ya Soilo-Salgaa.
Akizungumza Jumatatu afisini mwake, afisa anayesmamia mazingira katika kaunti hiyo ndogo Kennedy Kirwa, alisema shida ya utupaji taka kando ya barabara imekuwepo kwa muda mrefu sasa huku wafanyibiashara hao wakizidi kuchafua mazingira.
Aliongeza kuwa uchunguzi umebaini kuwa wanaotupa takataka hizo ni watu kutoka maeneo ya mbali na hutupa takataka hizo majira ya asubuhi ili wasitambulike.
“Kama idara ya mazingira,Tumefanya uchunguzi na tumebaini kuwa wanaotupa takataka ni watu kutoka maeneo ya mbali, na hivi karibuni tutawanasa, tumewawekea mtego,” Kirwa alisema.
Aidha Kirwa alitoa wito kwa wakaazi wa Rongai kuzingatia usafi wa mazingira kila wakati na kuwataka pia kuripoti watu wanaoharibu mazingira katika afisi yake.
Amesema watu wanaoharibu mazingira ni lazima wachukuliwe hatua kali za kisheria.