Vijana wa kukwangura na kuchimba mawe na kutengeneza kokoto katika timbo la mawe lililoko Daraja Mbili viungani mwa mji wa Kisii wamelalamikia maji ya mvua ambayo yanawatatiza msimu huu wa mvua inayoendelea kunyesha katika Kaunti hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana hao ambao hupata riziki yao kupitia kwenye shughuli hiyo ya kuponda mawe kuwa kokoto, walitaja mvua kuwa chanzo kikuu cha usumbufu ambapo walisema kuwa maji yamekuwa kero kwani yanajaa kwenye timbo hilo na kuwatatiza.

Wachongaji mawe hao kupitia kwa mwenyekiti wao Andrew Ondega, waliomba serikali ya kaunti kuwatafutia suluhu la maji hayo ambayo huwatatiza na kuwakwaza kutekeleza shughuli zao vilivyo.

Mwenyekiti wao Ondega pia aliitaka serikali ya Kaunti kuwajari kwa kuwanunulia vifaa muhimu vya kuwawezesha kufanya kazi yao kwa njia salama ambapo alisema kuwa wamekuwa wakiumizwa na mawe hayo kwenye viungo hasa macho.

"Wengine wetu tumeumizwa, na kupoteza jicho moja au mawili baada ya haya mawe kutuofyatukia machoni; tunamwomba gavana Ongwae atupe vizuizi vya macho imara hii miwani tunatumia haiko thabiti," mwenyekiti huyo alisema.