Wachungaji wa dini mbalimbali kutoka eneo la Masaba Kusini, Kaunti ya Kisii, wametoa wito kwa serikali kuwajumuisha katika bodi za miradi ya maendeleo.
Wakizungumza siku ya Jumatano katika Kanisa la Pentakosti la Kiamokama katika hafla ya kuchangisha pesa za ujenzi wa kanisa hilo, wachungaji hao, wakiongozwa na Mchungaji Ayuma Motari, walilalamikia kutengwa na viongozi wa kisiasa katika bodi za maendeleo.
Motari alisema kuwa hazina ya ustawi wa maeneo bunge al maarufu CDF, ya maeneo mengi nchini, hazijumuishi kanisa.
“Sisi kama viongozi wa makanisa pia tunafaa kujumuishwa katika bodi ya maendeleo ya maeneo yetu. Viongozi wa kisiasa pia wanahitaji mwelekeo wa Mungu hili kuzalisha matunda mema kwa watu wa mungu,” alisema Motari.
Mchungaji wa kanisa hilo la Kiamokama, Vincent Onkarora, aliwataka viongozi kuwa mstari wa mbele kulikuza na kueneza neno la Mungu wanapopata nafasi ya kuhutubia wananchi.
“Viongozi wetu walio opfisini kwa sasa wamesahau kuwa Mungu ndiye aliwapa wakati na nafasi hyo kuwa viongozi. Wanastahili kutoa shukrani kwa Mungu hili awape hekima na busara katika uongozi wao,” alisema Onkarora.
Mwanasiasa Benard Moseti, anayewania kiti cha ubunge cha Nyaribari Masaba aliahidi kutangamana na kufanya kazi pamoja na makanisa yote katika eneo hilo.
“Sisi tunamjua Mungu mmoja tu na basi tutafanya kazi na makanisa yote bila ubaguzi ili kuhakikisha usawa katika ustawi wa maendeleo ya eneo letu,” alisema Moseti.
Elijah Nyauma, ambaye pia ni mwanasiasa, aliwarai viongozi kuwa mfano wa kuigwa na waumini ili kufanikisha maendeleo katika eneo hilo.