Onyo limetolewa kwa wafanyibiashara wanaouza bidhaa zao kando kando mwa barabara katika eno la Obunga, Kaunti ya Kisumu kusonga umbali wa mita mia tano kutoka barabarani.
Onyo hiyo ilitolewa na mkuu wa trafiki katika kituo cha Polisi cha Chemelili, Peter Maina ambaye alisema kuwa mtu kukaa kando ya barabara ni sawa na kukaa karibu na shimo ndefu ambalo mtu anaweza kutumbukia ndani wakati wowote.
“Tunataka ieleweke vizuri na kila mmoja katika kila soko la eneo hili kwamba sheria za barabara haziruhusu yeyote kufanya shuhguli zake kando ya barabara. Tunataka mtu kuwa umbali wa mita mia tano. Hivyo basi wote wanaoendesha biashara kwenye maeneo ya barabara, tafadhali muondoke ili kuepuka hatari ya kukanyagwa na gari iwapo ajali inatokea,” alisema Maina.
Aidha, mkuu huyo wa trafiki alihoji kuwa hakujatokea kwa muda wa miaka mitano iliyopita kisa chochote cha gari kukosa mwelekeo na kuwadhuru wachuuzi kando kando mwa barabara, mbali na kile kilichotendeka mnamo mwaka wa 2010 ambapo mama mwenye umri wa makamo alikanyagwa na lori la kubeba mchanga lililokosa mwelekeo na kubingiria.
“Tunamshukuru Mungu kwa kuwa muda wa miaka mitano sasa bado hatujashuhudia kisa cha ajali katika eneo la soko hili, hivyo basi tunastahili kutahadhari kabla ya hatari kwani maisha yetu bado yanategemewa na wengi,” aliongeza.