Daktari mkuu katika hospitali ya Nyamira, Jack Magara amewaomba wakaazi wa kaunti ya Nyamira kushirikiana kwa kampeini ya kueneza hatari za ugonjwa wa kipindupindu.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Nyamira, daktari huyo aliwaonya wachuuzi wanaoendelea kuuza vyakula katika mji huo kutoendelea na biashara hiyo hadi wajulishwe na madaktari kuwa ugonjwa wa kibindubindu umeisha.
“Yeyote anayehitaji kufanya biashara hiyo ya kuuza vyakula mitaani hapa katika mji wa Nyamira sharti aende kwa hospitali apimwe na viwango vya usafi penye anafanyia viangaliwe ili kuruhusiwa kufanya biashara hiyo,”alidokeza daktari Magara.
Hii ni baada ya wachuuzi hao kuendelea na uuzaji wa vyakula hivyo katika kaunti ya Nyamira huku wakisema kuwa bila biashara hiyo hawawezi kuwasomesha watoto wao.
“Mimi nimekuwa nikifanya biashara hii ya kuuza vyakula hapa ili niweze kuwasomesha watoto wangu. Sasa nikiamrishwa kuacha biashara hii watoto wangu hawawezi kusoma kamwe maana hii ndio tegemeo langu katika maisha yangu,”alisema Beatrice Bosibori, mchuuzi.
Wachuuzi hao wameombwa kuzingatia usafi, kuwa na risiti za hospitali la sivyo wachukuliwe hatua kali za kisheria.
“Mkihitaji kufanya biashara hizo zingatia usafi angalau watu wasiathiriwe katika kaunti yetu,” alisema Magara.