Samaki wa kukaanga. [Picha/ blog.jasonmadrano.com]
Wanawake wanaofanya biashara ya kuuza samaki wa kukaanga mjini Kilifi wamedai kunyanyaswa kimapenzi na wavuvi ili waweze kuuziwa samaki kwa bei nafuu.Wanawake hao ambao hawakutaka kutajwa majina walisema kuwa wao hulazimika kushiriki ngono na wavuvi hao ili waweze kupata samaki wa kuuza.Baadhi ya wanawake hao wamesema kuwa wavuvi hao wanaendelea kuwanyanyasa kimapenzi kutokana na hali yao ya umaskini kwani wakati mwingine wao hukosa fedha za kununua samaki.“Umaskini wetu ndio unachangia sisi kushiriki ngono na wavuvi ili watupatie samaki bure. Hatuna pesa za kununua samaki hao,” alisema mmoja wa wanawake hao.Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumatatu, wachuuzi hao walisema kuwa wavuvi hao hukataa kuwauzia samaki wanawake wanaokataa kushiriki ngono nao.“Ukikataa kushiriki ngono na mvuvi basi hautauziwa samaki hao kwa bei nafuu,” alisema mchuuzi mmoja.Kwa upande wake, msimamizi wa wachuuzi hao wa samaki mjini Kilifi Rukia Mwanajuma alisema kuwa amepokea malalamishi kutoka kwa wanawake hao na kuwataka kukaidi wito wa wavuvi hao.“Nimepokea malalamishi mengi sana kuhusu kushiriki ngono na wavuvi kutoka kwa wanawake wengi sana. Ni jambo la kushangaza na kuhuzunisha sana,” alisema Rukia.Katika Kaunti ya Kwale, katibu wa miungano ya wavuvi Mwakiraa Mohamed amelalamikia idadi ndogo ya wakaazi wanaojihusisha na uvuvi licha ya kuwepo kwa raslimali muhimu ya bahari.Mohamed alisema kwamba vijana wengi wamekuwa na kasumba ya kwamba uvuvi ni kazi ya wazee huku wengi wakitegemea ajira kutoka kwa serikali.Katibu huyo ameitaka serikali kuwapatia vifaa vya kisasa ili kuimarisha viwango vya uvuvi hasa katika maeneo ya Vanga na Shimoni.