Idara ya afya na usafi wa umma wilayani Naivasha imeanzisha msako wa kuwanasa wachuuzi wanaouza chakula barabarani kutokana na kuongezeka kwa visa vya ugonjwa wa kipindupindu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Jumanne jioni, zaidi ya wachuuzi hamsini waliopatikana wakiuza chakula walinaswa kwenye oparesheni iliyofanyika kwenye makazi yote ya mji huo.

Afisaa mmoja wa idara hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa oparesheni hiyo ilianzia katika kitongoji duni cha Kihoto ambacho kimeathiriwa pakubwa na kuzuka kwa ugonjwa huo.

 "Msako huu utafanyika usiku na mchana na tutaendelea hadi pale visa vya mkurupuko huu wa kipindupindu vitapopunguka kabisa," aliongeza afisa huyo.

Kwa upande wake waziri wa maswala ya afya wa kaunti ya Nakuru Dr. Mungai Kabii alisema kuwa kesi nyingi zinazoripotiwa mjini Naivasha zimetokana na kuwepo kwa wasafiri wengi wanaopitia mji huo.

Akizungumza  Jumatano, Kabii alihoji kuwa imekuwa vigumu kuweza kuwadhibiti wanaoingia mji huo na kuondoka na kuwataka wakenya kuzingatia usafi bora.

"Ningependa kuwahimiza wakenya na haswa wakaazi wa Naivasha kuzingatia usafi ili kuepuka maafa," alisema Kabii.